Kikosi cha pili cha wanajeshi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kilichokuwa kimetumwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kusaidia jeshi la serikali dhidi ya waasi wa M23, kimerejea nyumbani kupitia Rwanda.
Majira ya saa mbili usiku siku ya Jumapili, Mei 4, magari ya mizigo yaliyojaa vifaa vya kijeshi yaliondoka wilayani Rubavu.
Ifikapo saa tatu na dakika hamsini usiku, msafara huo ulikuwa umefika mjini Musanze, na hivyo kuna uwezekano mkubwa kuwa ulifika Kigali saa sita usiku.
Picha zilizopigwa na mwandishi wa BWIZA zilionyesha angalau malori makubwa 35 yakiwa na vifaa vya kijeshi vya SADC, yakisindikizwa na polisi na jeshi la Rwanda.
Hili ni kundi la pili kuondoka, likifuatia lile la kwanza lililoondoka Alhamisi, Mei 2, 2025.
Mwanzoni mwa Januari mwaka huu, wanajeshi wa SADC walikuwa wamezingirwa mjini Goma baada ya waasi wa M23 kuuteka mji huo na kuwafurusha wanajeshi wa serikali na washirika wao.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Balozi Olivier Nduhungirehe, alisema hivi karibuni kuwa uwepo wa wanajeshi kutoka Afrika Kusini, Malawi na Tanzania mashariki mwa Congo ulikuwa ukichochea hali ya mvutano zaidi.
Akasema: “Rwanda inatoa njia salama na kusindikiza kwa amani magari ya kijeshi ya SAMIDRC yanayovuka mashariki mwa DRC kupitia Rwanda kuelekea Tanzania pamoja na vifaa vyao.”
“Uwepo wa kudumu wa wanajeshi wa SAMIDRC ulikuwa ukiongeza hali ya mvutano, na kuanza kwa kurudi kwao ni hatua nzuri katika kuunga mkono jitihada za amani zinazoendelea.”
SADC ilikuwa imetuma vikosi vyake Congo mwishoni mwa 2023 kusaidia mapambano yaliyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu.
Walichukua nafasi ya vikosi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) vilivyofukuzwa na serikali ya Congo kwa kukataa kupambana moja kwa moja na waasi wa M23.


