Ripoti iliyotolewa Jumanne na shirika la Human Rights Watch (HRW) imetaja waasi wa M23 kuwa waliwaua angalau raia 21 katika kipindi cha siku mbili tu mwezi Februari, katika jiji la Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ripoti hiyo, inayohusu matukio ya tarehe 22 na 23 Februari, inaonesha kiwango cha ukandamizaji na mauaji yaliyofanyika wakati ghasia zikiongezeka.
HRW ilisema: “Viongozi na wapiganaji waliotoa maagizo au kutekeleza unyama huu moja kwa moja lazima wawajibishwe.”
Waasi wa M23 wamechukua udhibiti wa miji miwili mikubwa, Goma na Bukavu, tangu mashambulizi yaanze Januari. Mashambulizi hayo yamesababisha maelfu ya vifo na maelfu kuhama makazi.
Ripoti ya HRW inasema kuwa Februari 22, raia 21 wakiwemo wanaume 6 na mwanamke 1, waliuawa kwa kupigwa risasi kichwani karibu na kambi ya kijeshi ya Katindo huko Goma. Mashahidi walieleza kuwa M23 ndio waliohusika.
Kwenye matukio mengine, M23 inasemekana waliua watu na kutupa miili yao kwenye eneo la ujenzi, takribani mita 100 kutoka kambi ya jeshi. Miongoni mwa waliouawa alikuwa mvulana wa miaka 15, aliyetekwa nyumbani kwao na baadaye kupatikana amekufa, kulingana na jamaa yake na jirani.
Eneo la Kasika, Goma lilishambuliwa kwa sababu lilikuwa na ngome za jeshi la Congo hapo awali.
Mnamo Februari 23, ghasia ziliendelea ambapo waasi wa M23 walikusanya vijana wapatao 20 katika uwanja wa michezo wa karibu. Mmoja wa mashahidi alisema waasi hao walidai vijana hao ni wanajeshi wa serikali. Watatu waliokimbia walipigwa risasi na kuuawa.
Kiongozi wa M23, Bertrand Bisimwa, aliliambia shirika la Reuters kuwa watachunguza tuhuma hizo:
“HRW inatupa nafasi ya kujitathmini. Tunaiheshimu taasisi hiyo, ingawa baadhi ya madai ya nyuma yalikuwa ya uongo.”
HRW iliongeza kuwa wafanyakazi wa afya walithibitisha kuwa zaidi ya miili 50 ilikusanywa Kasika ndani ya siku mbili.
Mashirika mengine kama Amnesty International yameripoti pia kuwa M23 walivamia hospitali huko Goma mwezi Machi wakiwatafuta wanajeshi waliojeruhiwa na kuwateka watu 130, wakiwemo wahudumu wa afya. Wengi waliteswa na baadhi bado hawajulikani waliko.

