Habari kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinaonyesha kuwa waasi wa M23 wanaendelea kuimarisha vikosi vyao katika maeneo mbalimbali ya Masisi na Walikale.
Ripoti zinaeleza kuwa mwishoni mwa wiki iliyopita, kundi hilo liliongeza kwa kiwango kikubwa wanajeshi na vifaa vya kijeshi katika maeneo tofauti.
Katika maeneo ya Masisi–Nyabyondo–Kasopo na Nyabyondo–Kinyumba huko Masisi, inasemekana kuwa Ijumaa iliyopita magari mengi yaliwasili yakisafirisha wanajeshi na vifaa.
Jioni hiyo, takribani malori saba ya kijeshi ya aina ya Kamaz yaliripotiwa kufika katikati ya Nyabyondo yakiwa na wanajeshi, na siku ya Jumamosi yakafuatwa na malori mengine manne.
Mbali na Masisi, M23 pia iliongeza wanajeshi na vifaa katika maeneo ya Kashebere na Kibati ndani ya Wilaya ya Walikale.
Katika wilaya hiyo hiyo, harakati za M23 na vifaa vyao vilionekana katika maeneo ya Kalembe–Kalonge–Pinga. Ripoti zinaeleza kuwa katika mkutano na wakazi wa Kalembe, viongozi wa M23 waliwaambia kuwa wanapanga kushambulia na kuteka mji wa Pinga.
Pinga ni mji ulioko katika Wilaya ya Walikale, zaidi ya kilomita 150 kaskazini-magharibi mwa Goma.
Pia imeripotiwa kuwa kundi hilo limeanza kuelekeza silaha zake nzito kuelekea eneo la Mpeti.
Kwa sasa kuna hofu kubwa kwamba mapigano makali yanaweza kuanza tena kati ya M23 na jeshi la serikali katika eneo la magharibi ya Mkoa wa Kivu Kaskazini, baada ya zaidi ya miezi miwili ya utulivu.

