Serikali ya Marekani imewaonya raia wake wasisafiri kwenda katika mataifa 21 duniani, likiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
DRC na mataifa mengine yaliyotajwa yamewekwa katika ngazi ya 4 ya onyo — ambayo ni kiwango cha juu kabisa cha hatari.
Serikali ya Marekani inasema kuwa nchi zilizo katika kiwango hiki ni hatari sana, na pia inakiri kuwa haina uwezo wa kuwasaidia raia wake ipasavyo ikiwa watakumbwa na dharura wakiwa huko.
Ilitoa ujumbe kwa raia wake ikisema:
“Maeneo haya ni hatari sana, hivyo unaweza kujiweka kwenye hatari kubwa ukisafiri huko.”
Nchi zilizoorodheshwa ni zile zinazokumbwa na vita, machafuko, au ambazo zina uhusiano wa mvutano na Marekani.
Mbali na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mataifa mengine ni:
Afghanistan, Belarus, Myanmar, Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Haiti, Iran, Iraq, Lebanon, Libya, Mali, Korea Kaskazini, Urusi, Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Syria, Ukraine, Venezuela na Yemen.


