Jumanne, Aprili 22, zaidi ya polisi 180 walioko katika makao makuu ya Polisi ya Rwanda mjini Kacyiru walijitolea kuchangia damu kwa hiari ili kusaidia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo ya dharura hospitalini.
Msemaji wa Polisi ya Rwanda, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Boniface Rutikanga, alisema kwamba tukio hili ni sehemu ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Polisi na Kituo cha Taifa cha Afya cha Rwanda (RBC), pamoja na dhamira yao ya kuboresha maisha ya jamii.
Alisema: “Kwetu sisi Polisi, kuchangia damu si tu kutimiza makubaliano na RBC, bali pia ni sehemu ya jukumu letu la kulinda maisha na kuhakikisha ustawi wa wananchi. Hakuna usalama wa kweli ikiwa watu wanahangaika na magonjwa.”

Daktari Andre Munyemana kutoka RBC, anayesimamia kitengo cha damu, aliipongeza Polisi ya Rwanda kwa ushirikiano wao wa mara kwa mara na kuwashukuru askari waliojitoa kwa moyo kusaidia jamii.
Alisema: “Kuchangia damu ni tendo la huruma na utu. Bila damu ya dharura, maisha ya watu wengi yangepotea. Bidii na moyo wa kujitolea ulioonyeshwa na polisi unatakiwa kuwa mfano kwa kila mwananchi.”
Dkt. Munyemana alitoa wito kwa kila Mnyarwanda kutambua kuwa kuchangia damu ni wajibu wa kila mmoja, akisisitiza kuwa mtu yeyote anaweza kuhitaji damu kwa ajili yake au jamaa wakati wowote.


