Polisi wa Brazil wamesema wamefanikiwa kuzuia shambulio la bomu lililokuwa limepangwa kufanyika katika tamasha la Lady Gaga kwenye ufukwe wa Copacabana, Rio de Janeiro, siku ya Jumamosi.
Polisi wa kiraia wa Jimbo la Rio de Janeiro, wakishirikiana na wizara ya haki, walisema washukiwa walikuwa wamewaajiri baadhi ya watazamaji wa tamasha hilo kushambulia kwa mabomu ili kujitangaza kupitia mitandao ya kijamii.

Polisi walieleza kuwa mtu aliyepanga shambulio hilo na kijana aliyekuwa akishirikiana naye walikamatwa, kwa mujibu wa ripoti ya BBC.
Timu ya Lady Gaga ilisema walikuwa wanajua kuhusu mipango ya shambulio hilo lakini walitangaza hilo kwa vyombo vya habari asubuhi ya Jumapili baada ya tamasha kumalizika.
Zaidi ya watu milioni mbili walihudhuria tamasha hilo la bure, lililodhaminiwa na halmashauri ya jiji la Rio.

Polisi walisema kikundi kilichopanga shambulio hicho kimekuwa kikieneza maneno ya chuki, hasa dhidi ya watoto, vijana na watu wa LGBTQ+.
Mshukiwa mkuu alikamatwa kwa kosa la kumiliki bunduki kinyume cha sheria katika jimbo la Rio Grande do Sul, huku kijana mwenzake akitiwa mbaroni kwa kosa la kumiliki picha za matusi zinazohusisha watoto mjini Rio.


