Rais Paul Kagame yuko mjini Algiers, Algeria, ambako alianza ziara rasmi ya kikazi Jumanne hii tarehe 3 Juni.
Habari za ziara hiyo zilithibitishwa na vyanzo mbalimbali, ikiwemo Ubalozi wa Algeria ulioko Paris, Ufaransa.
Kupitia akaunti yake rasmi ya X, ubalozi huo ulitangaza kuwa Rais Kagame alitembelea nchi hiyo ya Afrika Kaskazini kufuatia mwaliko kutoka kwa Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune.
Ujumbe huo ulisema: “Kwa mwaliko wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri, Abdelmadjid Tebboune, Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame, ameanza ziara ya siku mbili nchini Algeria.”
Ziara hiyo ya Kagame inafuatia mkutano na mazungumzo aliyofanya na Rais Tebboune mwezi Desemba mwaka jana.
Marais hao wawili walikutana mjini Nouakchott, Mauritania, walipokuwa wakihudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika kuhusu elimu na ujuzi wa vijana kwa ajili ya ajira.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Ikulu ya Rwanda wakati huo, walijadili juu ya “kuimarisha ushirikiano mzuri kati ya nchi hizo mbili katika maeneo muhimu kama vile elimu, ulinzi na usalama.”
Pia walijadili maeneo mapya ya ushirikiano, yakiwemo kilimo na miundombinu.
Rais Kagame alitembelea Algeria mara ya mwisho mwezi Juni mwaka 2015.
Katika ziara hiyo, alikutana na viongozi wa juu wa Algeria na kusisitiza kuwa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili unapaswa kuwanufaisha wananchi wa pande zote na Afrika kwa ujumla.
Pia aliweka shada la maua katika mnara wa kumbukumbu wa mashujaa waliofariki wakati wa vita vya uhuru wa Algeria.
Algeria na Rwanda zimekuwa na uhusiano mzuri tangu mwaka 1978, na mwaka 2014 Algeria ilifungua ubalozi wake mjini Kigali.
Agosti 2023, Rais Kagame alipokea hati za utambulisho kutoka kwa mabalozi 12 wapya walioteuliwa kuwakilisha nchi zao nchini Rwanda, wakiwemo wa Algeria, Mohamed Mellah, ambaye makao yake ni Kigali.
Mambo mengine yanayodumisha uhusiano wa mataifa haya mawili ni uanachama wao katika mashirika kama vile Umoja wa Afrika (AU), NEPAD, Umoja wa Mataifa (UN), na Jumuiya ya Nchi zinazozungumza Kifaransa (OIF).
Algeria ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kusaini mkataba wa kuanzisha Soko Huru la Bara la Afrika (AfCFTA), ulioidhinishwa mjini Kigali mnamo Machi 2018.
Mwaka 2016, katika Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Kigali (KICD) uliofanyika mjini Algiers, Mke wa Rais, Bi Jeannette Kagame, alitunukiwa tuzo kwa mchango wake mkubwa katika kupambana na ukatili wa kijinsia na kuinua wanawake na wasichana kupitia shirika la Imbuto Foundation.
Tangu mwaka 1982, Rwanda na Algeria zimesaini mikataba mbalimbali kuhusu uchumi, ustawi wa jamii, utamaduni, na ushirikiano.
Pia zimekubaliana kuongeza nguvu katika sekta za afya, biashara, uwekezaji, usalama, na elimu.

