Rais Paul Biya wa Cameroon ametangaza rasmi kuwa atawania tena urais kwa muhula wa nane katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Akiwa na umri wa miaka 92, Biya ndiye rais mzee zaidi anayeongoza duniani kwa sasa.
Kiongozi huyu ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 43, alithibitisha azma yake kupitia ujumbe kwenye ukurasa wake wa X (zamani Twitter), akiwambia wananchi:
“Mimi ni mgombea katika uchaguzi wa urais. Ninawahakikishia kuwa lengo langu ni kuwahudumia kwa dhati katika kutatua matatizo yanayotukumba kwa haraka.”
Endapo atachaguliwa tena, Biya ataendelea kuongoza hadi atakapofikisha miaka 100. Alianza kuongoza mwaka 1982 baada ya kumrithi Ahmadou Ahidjo, aliyeng’atuka.
Tangu mwaka jana, wafuasi wa chama chake cha Rassemblement démocratique du peuple camerounais (RDPC) na waungaji mkono wake wamekuwa wakimsihi agombee tena, ingawa vyama vya upinzani na mashirika ya kijamii wametaka astaafu kwa madai kuwa utawala wake mrefu umechelewesha maendeleo ya kiuchumi na demokrasia nchini humo.
Biya huonekana hadharani mara chache sana na kwa kawaida huishi Uswisi. Mwaka jana, alipotea machoni mwa umma kwa zaidi ya siku 42, na kusababisha uvumi kwamba huenda amefariki, hali iliyolazimu serikali kukanusha na kupiga marufuku majadiliano kuhusu afya yake.


