Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda, Balozi Olivier Nduhungirehe, alizungumza kwa simu na Naibu Waziri katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Dkt. Mohammed bin Abdulaziz Al-Khulaifi, kujadili ujumbe wa rambirambi wa Rwanda kwa watu wa Qatar kufuatia mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na Iran.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Nduhungirehe alimpa mwenzake wa Qatar ujumbe wa pole na mshikamano kutoka Rwanda kwa watu wa Qatar, huku akilaani vikali mashambulizi ya makombora yaliyoelekezwa kwenye kambi ya jeshi la anga la Marekani ya Al Udeid, iliyoko Qatar.
Mnamo Jumatatu, tarehe 23 Juni 2025, Iran ilitangaza kuwa ilifanya mashambulizi dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani zilizoko Qatar na Iraq, kama kisasi kwa mashambulizi yaliyofanywa dhidi yake na Marekani mnamo Jumapili, tarehe 22 Juni 2025.
Mashambulizi hayo yalitokea wakati Qatar tayari ilikuwa imefunga anga lake kwa tahadhari, kufuatia vitisho kutoka Iran. Qatar ilisema kuwa mashambulizi hayo hayakusababisha uharibifu wowote kwani makombora hayo yalizuiliwa angani kabla hayajafika ardhini, kutokana na mifumo ya ulinzi wa anga.
Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Qatar, ilielezwa kuwa mifumo ya ulinzi wa anga ya taifa hilo ilifanikiwa kuzuia mashambulizi ya makombora kutoka Iran dhidi ya kambi ya Marekani ya Al-Udeid, na hakuna mtu aliyejeruhiwa.
Iran pia ilirusha makombora kuelekea kambi ya Ain al-Assad nchini Iraq, ambako kuna wanajeshi wa Marekani, kulingana na afisa mmoja mwandamizi wa usalama nchini Iraq aliyenukuliwa na shirika la habari la Uingereza, Associated Press, kwa sharti la kutotajwa jina.


