Mlipo wa bomu unaoshukiwa kutokea Munyonyo, umevuruga sherehe za maadhimisho ya Siku ya Mashahidi katika mji mkuu wa Uganda, Kampala.
Asubuhi ya Jumanne hii, mlipuko mkubwa ulisikika karibu na Kanisa la Mashahidi la Munyonyo, ambapo watu kutoka maeneo mbalimbali walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya maadhimisho ya kila mwaka ya Siku ya Mashahidi.
Ripoti za awali zinaonyesha kuwa mabaki ya mwili wa binadamu yalipatikana eneo la tukio, pamoja na sehemu za pikipiki iliyoharibika vibaya, ishara kuwa huenda aliyeuawa alikuwa sehemu ya waliosababisha mlipuko huo.
Maafisa wa usalama, wakiwemo wanajeshi, polisi na wataalamu wa mabomu, walifika haraka na kufunga eneo hilo kwa uchunguzi zaidi. Wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi wanachunguza eneo la tukio ili kubaini chanzo halisi cha mlipuko.
Jeshi la Uganda (UPDF) lilitangaza kuwa kikosi chake maalum cha kupambana na ugaidi kilimuua magaidi wawili waliokuwa na silaha ambao wanadaiwa kuhusika katika tukio hilo mapema asubuhi.
Katika taarifa yake, UPDF ilisema:
“Operesheni hii iliongozwa na taarifa sahihi za kiintelijensia. Vikosi vya usalama vinaendelea kuwa katika hali ya tahadhari ili kuhakikisha maadhimisho yanaendelea salama bila kikwazo.”
Iliongeza:
“Wananchi wanahimizwa kudumisha utulivu lakini pia wawe waangalifu, na kutoa taarifa kuhusu mtu, kitu au tukio lolote la kushukiwa kwa vyombo vya usalama mara moja.”
Mlipuko huu umetokea wakati ambapo hatua kali za kiusalama zilikuwa tayari zimechukuliwa Kampala, kwa sababu ya maadhimisho ya Siku ya Mashahidi, siku ya kukumbuka Wakristo 45 waliouawa kati ya 1885 na 1887.
Maafisa wa usalama walikuwa tayari wameonya kuhusu tishio la mashambulizi kutoka kwa makundi ya kigaidi yanayonuia kuvuruga mikusanyiko ya kidini na ya kijamii.

