Urusi imetangaza kwamba imezuia shambulio la ndege zisizo na rubani lililokuwa likielekezwa mjini Moscow wakati jiji hilo linaendelea na maandalizi ya sherehe kubwa za kijeshi zitakazohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kimataifa.
Jumatatu, Meya wa Moscow, Sergei Sobyanin, alisema kwamba mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi iliangusha “drones nne zilizokuwa zikielekea Moscow.”
Shambulio hilo linaonekana kuwa lililenga kuvuruga maandalizi ya sherehe za Siku ya Ushindi, siku ya kumbukumbu ya kumalizika kwa kile Urusi huuita Vita Kuu ya Uzalendo, inayojulikana kimataifa kama Vita ya Pili ya Dunia, inayoadhimishwa Mei 9.
Rais Vladimir Putin alikuwa ameomba kuwe na usitishaji wa mapigano kwa saa 72 kuanzia Mei 8 ili kutoa nafasi kwa sherehe hizo, kwa mujibu wa taarifa ya Al Jazeera.
Hata hivyo, Ukraine ilijibu kwa kupendekeza usitishaji wa mapigano wa siku 30 kwa lengo la kufanikisha kusitisha vita vilivyoanza Februari 2022.
Katika ujumbe alioweka kwenye Telegram, Sobyanin alithibitisha kwamba hakuna taarifa za majeruhi wala uharibifu zilizopatikana.
Hata hivyo, shambulio hilo lilisababisha ndege kusitisha safari katika Uwanja wa Ndege wa Domodedovo mjini Moscow. Mamlaka ya anga ya Urusi, Rosaviatsia, ilithibitisha kuwa safari za anga zilisitishwa kwa dakika 90 usiku huo ili kuhakikisha usalama wa anga.
Kwingineko, maafisa wa Urusi walitangaza kuwa drones 17 ziliangushwa katika Mkoa wa Bryansk na zingine tano juu ya Kaluga.


