Idara ya Upelelezi ya Rwanda (RIB) imethibitisha kuwa imekamata mwanasiasa Victoire Ingabire Umuhoza, baada ya ombi kutoka kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu kuanzisha uchunguzi dhidi yake.
Kupitia chapisho kwenye akaunti yake ya X (zamani Twitter), RIB ilisema kuwa Ingabire, kiongozi wa chama cha kisiasa Dalfa-Umurinzi kisichotambuliwa rasmi nchini Rwanda, yuko mikoni mwao kwa sasa.
“RIB, kwa agizo la Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, mnamo tarehe 19 Juni 2025, ilianza uchunguzi dhidi ya Victoire Ingabire Umuhoza, kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi dhidi ya Sibomana Sylvain na wenzake, ili aweze kufikishwa mahakamani.”
RIB imeeleza zaidi kuwa Ingabire na washirika wake wanachunguzwa kwa makosa ya “kuunda kikundi cha kihalifu na kupanga matendo ya kuchochea ghasia miongoni mwa umma.”
Kwa sasa, mwanasiasa huyo anazuiliwa katika Kituo cha RIB cha Remera, akisubiri kuwasilishwa kwa Mwendesha Mashtaka.
Kukamatwa kwake kunakuja baada ya kufika mbele ya Mahakama Kuu siku ya Alhamisi, kufafanua tuhuma dhidi ya wanachama wa chama chake wanaodaiwa kuhudhuria mafunzo ya kumwondoa serikali bila kutumia nguvu za kijeshi.
Mahakama ilimuita Ingabire baada ya kutajwa mara kwa mara na upande wa mashtaka katika vikao vya awali, wakimhusisha moja kwa moja na mafunzo hayo.
Alipotoa maelezo yake, Ingabire alikiri kuwajua washukiwa tisa, lakini alikanusha vikali kuhusika kwa namna yoyote katika mafunzo hayo au kushiriki chama chake, hasa kwa kuwa chama hicho hakitambuliwi rasmi nchini Rwanda.
Baada ya kikao cha faragha cha saa mbili, mahakama iliamua kuwa maelezo aliyotoa hayatoshi na kuna ushahidi wa msingi unaohitaji uchunguzi wa kina.
Jaji aliyekuwa akiongoza kesi hiyo aliamuru Mwendesha Mashtaka kuanzisha uchunguzi, na kuwasilisha matokeo kwa mahakama.
Mahakama Kuu ya Kigali imeagiza kwamba uchunguzi huo ukamilike ndani ya wiki mbili, kuanzia Ijumaa tarehe 20 Juni 2025.


