Waziri Mkuu wa Mongolia, Luvsannamsrain Oyun-Erdene, amejiuzulu baada ya picha za mwanawe akiwa anaishi maisha ya kifahari wakati wa likizo kusambaa mitandaoni.
Miongoni mwa picha hizo, kulikuwa na mpenzi wa mwanawe akiwa na mkoba wa gharama kubwa wa Dior, jambo lililowakera raia wengi na kusababisha uchunguzi wa tuhuma za ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.
Wananchi wengi walihoji jinsi familia ya Waziri Mkuu ilivyoweza kuishi maisha ya anasa kiasi hicho, na hali hiyo ilichochea maandamano makubwa, hasa ya vijana, waliodai ajiuzulu kwa muda wa wiki mbili mfululizo.
Jumanne hii, Bunge lilimpigia kura ya siri ambapo wabunge 44 kati ya 88 walimuunga mkono huku 38 wakimpinga. Ili abaki madarakani, alihitaji kura zisizopungua 64.
Oyun-Erdene alikana madai yote, akisema ni uwongo uliolenga kumchafua. Hata hivyo, Tume ya Taifa ya Kupambana na Ufisadi ilikuwa tayari ikifuatilia matumizi ya kifedha ya familia yake kwa muda.
Mongolia bado inakumbwa na tatizo sugu la ufisadi. Shirika la Transparency International limeiweka katika nafasi ya 114 kati ya mataifa 180 duniani kwa suala la utawala bora.

