image-1747162787

Trump Aondoa Vikwazo kwa Syria, Kufungua Mlango wa Ushirikiano Mpya

Sangiza iyi nkuru

Rais wa Marekani Donald Trump, siku ya Jumanne, alitangaza kwamba ameondoa vikwazo ambavyo Marekani ilikuwa imeviwekea Syria.

Trump alitoa tangazo hilo akiwa Riyadh, Saudi Arabia, alipokuwa akihudhuria mkutano wa uwekezaji.

Alisema: “Ninaamuru vikwazo dhidi ya Syria viondolewe, ili kuwapa nafasi ya kuwa taifa lenye mafanikio. Huu ni wakati wa maridhiano. Vikwazo vyote vinaondolewa. Kila la heri Syria — tuonyesheni jambo la kipekee.”

Trump alisema amefikia uamuzi huo baada ya mashauriano na Mwana Mfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, pamoja na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.

Viongozi hao wawili wamekuwa wakishinikiza kwa muda mrefu kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Syria.

Baada ya kuondolewa kwa vikwazo hivyo, Rais Trump anatarajiwa kukutana na Rais wa Syria, Ahmed al-Sharaa, siku ya Jumatano.

Sharaa, ambaye alikuwa kiongozi wa zamani katika kundi la kigaidi la Al-Qaeda, alitwaa madaraka mwaka jana baada ya kumng’oa Bashar al-Assad.

Mkutano kati ya Trump na Sharaa umepangwa kufanyika Riyadh.

Rais wa Marekani alisema vikwazo hivyo vilitimiza malengo yake, lakini sasa ni wakati wa Syria kusonga mbele.

Aliongeza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, anaratibu hatua zinazofuata wiki hii na atakutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Asaad al-Shibani.

Shibani alisema kuwa Syria iko tayari kuwa na uhusiano na Marekani “unaotegemea heshima, uaminifu na maslahi ya pamoja.”

Vikwazo vya awali vilikuwa vimeiondoa Syria katika mfumo wa fedha wa kimataifa, na kufanya uwekezaji wa nje kuwa mgumu sana.

Trump alibainisha kuwa mara baada ya kuondoa vikwazo, Marekani na Saudi Arabia walikubaliana mkataba wa uwekezaji wa thamani ya dola bilioni 600.

Soma Izindi Nkuru

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *