Mahakama Kuu ya Afrika Kusini imemhukumu Kelly Smith kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuuza binti yake wa miaka sita, Joshlin Smith, katika kesi iliyogusa nyoyo za watu wengi tangu msichana huyo apotee mwaka jana.
Kelly Smith, mpenzi wake Jacquen Appollis, na mshirika wao Steveno Van Rhyn wote walikutwa na hatia ya utekaji na usafirishaji wa mtoto.
Kwa mujibu wa mashahidi waliotoa ushahidi mahakamani, Smith alikiri kumtoa binti yake kwa sangoma (mganga wa kienyeji) kwa malipo ya randi 20,000 (zaidi ya milioni 1.5 za Rwanda), kwa madai kwamba mtoto huyo alihitajika kwa ajili ya “macho na ngozi yake.”
Licha ya uchunguzi wa muda mrefu uliofanywa na polisi, hadi sasa haijulikani Joshlin yuko wapi.
Akisoma hukumu siku ya Alhamisi, Jaji Nathan Erasmus alisema kwamba uraibu wa dawa za kulevya haukuwa sababu ya kupunguza adhabu yao.
Jaji Erasmus alisema: “Sioni sababu yoyote ya kuwapa adhabu nyepesi kuliko adhabu kali kabisa inayowezekana.”
Kwa kosa la utekaji, kila mmoja wao alipata kifungo cha miaka 10, kando na kifungo cha maisha kwa kosa la kusafirisha mtoto.
Kesi hii imeonyesha wazi ukatili wa biashara haramu ya binadamu nchini Afrika Kusini, na imesababisha wito mpya kwa serikali na wananchi kuhakikisha ulinzi zaidi kwa watoto, hasa katika familia zinazokumbwa na umaskini na matumizi ya dawa za kulevya.
Hadi sasa, hatima ya Joshlin Smith haijulikani.


