Joseph Kabila Akutana na Viongozi wa M23
Joseph Kabila Kabange, ambaye amekaa takribani wiki moja katika jiji la Goma, alikutana siku ya Ijumaa tarehe 30 Mei na viongozi wa muungano wa Alliance Fleuve Congo unaojumuisha kundi la waasi la M23.
Miongoni mwa waliokutana naye ni Corneille Nangaa, mratibu wa Alliance Fleuve Congo, pamoja na Bertrand Bisimwa, ambaye ni rais wa kundi la M23.
Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Nangaa alisema kuwa mkutano huo ulikuwa na lengo la “kuweka na kuimarisha amani ya kudumu, umoja wa kitaifa na mshikamano wa kudumu.”
Kabla ya mkutano huu na viongozi wa M23, Kabila alikuwa tayari amekutana na wawakilishi wa dini pamoja na viongozi wa jadi kutoka jimbo la Kivu Kaskazini.
Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), aliyeongoza kati ya 2001 na 2019, amekuwa Goma tangu Jumapili iliyopita baada ya kurejea kutoka kusini mwa Afrika ambako alikuwa amekimbilia.


