Alhamisi, tarehe 29 Mei 2025, Rwanda iliungana na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa.
Tangu Rwanda ilipoanza kushiriki katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa mwaka 2004, imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha amani na usalama duniani, na kwa sasa ni nchi ya pili kwa idadi kubwa ya wanajeshi wanaotumwa.

Katika maadhimisho haya ya Siku ya Walinda Amani, medali mbili za Dag Hammarskjöld zilitolewa kwa heshima ya marehemu Sajenti Meja Fiston Murwanashyaka na Koplo Eliakim Niyitegeka waliopoteza maisha wakihudumu katika kazi za kulinda amani.
Medali hizo zilipokelewa na Balozi wa Rwanda katika Umoja wa Mataifa, Martin Ngoga.

Balozi Ngoga pamoja na Mshauri wa Kijeshi, Kanali Deo Mutabazi, walisema kuwa medali hizo ni ishara ya kujitolea kwa hali ya juu katika kuwalinda raia wasiojiweza na kuhakikisha amani, hata nje ya mipaka ya Rwanda.

Medali ya Dag Hammarskjöld hutolewa na Umoja wa Mataifa kwa askari, polisi au raia waliopoteza maisha wakiwa kwenye jukumu la kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa.

Medali hiyo inaitwa kwa heshima ya Dag Hammarskjöld, Katibu Mkuu wa pili wa Umoja wa Mataifa, aliyefariki katika ajali ya ndege mwezi Septemba 1961 katika eneo linalojulikana leo kama Zambia.


