Gavana wa Kijeshi wa Mkoa wa Kivu Kaskazini, Luteni Jenerali Johnny Luboya, amesema kuwa wanajeshi wa Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) wanauawa na waasi wanaoongozwa na Thomas Lubanga kwa sababu wamepoteza morali ya kupigana.
Alisema haya Ijumaa, Mei 30, alipokuwa anaeleza matatizo mbalimbali yanayolikumba jeshi la Congo katika mapambano dhidi ya makundi yenye silaha huko Ituri.
Miongoni mwa makundi hayo ni CRP linaloongozwa na Lubanga, ambalo limeanzisha mashambulizi dhidi ya majeshi ya serikali.
Katika mkutano na wanahabari, Jenerali Luboya alithibitisha kuwa wanajeshi wengi wa FARDC wanauawa na waasi hao.
Alisema: “Mwanajeshi aliye mstari wa mbele, kama sasa tunavyopigana na CRP-M23 — waasi wa Thomas Lubanga ambaye sasa ni mshirika wa M23 — wanajeshi wetu wanakufa.”
Miongoni mwa matatizo anayosema yanapunguza morali ya jeshi ni suala la wajane wa askari waliouawa, ambao wamelalamikia kutolipwa fidia kwa miaka mingi.
Luteni Jenerali Luboya alisema kuwa suala hili liliwasilishwa mara kadhaa kwa ukaguzi mkuu wa jeshi, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.
Alisema: “Tuna tatizo la kuwatambua wajane. Tumehangaika kwa miaka mingi kuwatambua. Hivi karibuni, timu kutoka ukaguzi mkuu walikuja hapa kwa shughuli hiyo, lakini kila wanapokuja, hakuna kinachofanyika.”
Aliongeza kuwa hali hii inawavunja moyo wanajeshi walioko vitani.
Alisema: “Kama mwanajeshi anapigana lakini anajua kuwa wajane hawatalipwa, kwa nini ajitoe muhanga? Anaweza kusema, ‘nikifa, watoto wangu wataachwa kama wale wa mashariki.’ Hii inawakatisha tamaa wanajeshi, hasa walioko mstari wa mbele. Kwa nini waendelee kupigana ilhali wanajua familia zao hazitapewa msaada wowote?”
Luboya pia alifichua kuwa baadhi ya wajane wameanza kuandamana wakiwa uchi, na akaeleza kuwa kuna upungufu mkubwa wa wanajeshi — suala alilowasilisha kwa Rais Félix Tshisekedi lakini bado halijapatiwa suluhisho.
Aliongeza: “Mnajua tuko eneo la vita, hatufai kuvurugwa au kuvunjika moyo kwa sababu ya matatizo haya. Jeshi halipaswi kuwa na matatizo yaleyale kila wakati.”
“Nilipokuwa hapa mara ya kwanza Rais alipokuja, nilimweleza wazi kuhusu uhaba wa wanajeshi. Watu wanasema chochote, lakini matokeo tumeona. Naamini makamanda walioko Goma waliona nilichokuwa nazungumzia.”
Gavana wa Kijeshi wa Ituri alisema haelewi kwa nini kikosi chenye uwezo wa kuwa na wanajeshi 1,200 huwa na 300 au 400 pekee — bila yeyote kuwajibika.
Aliongeza kuwa wanajeshi walioko vitani wanakabiliwa na njaa kali, wakila mara 15 tu kwa mwezi, licha ya fedha kutengwa na Wizara ya Ulinzi — jambo linalowakatisha tamaa zaidi.


