11-og_image

Ajali ya Ndege ya Kijeshi Yaua Wanajeshi Watano wa Uganda Mogadishu

Sangiza iyi nkuru

Wanajeshi watano wa Jeshi la Ulinzi la Uganda (UPDF) wamefariki dunia katika ajali ya ndege ya kijeshi iliyotokea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mogadishu, nchini Somalia, siku ya Jumatano, tarehe 2 Julai 2025.

Ndege hiyo ilikuwa kwenye operesheni ya Ujumbe wa Umoja wa Afrika wa Usaidizi na Utulivu nchini Somalia (AUSSOM) ilipokuwa ikijaribu kutua uwanjani, lakini ikapata ajali mbaya, kulingana na msemaji wa UPDF, Brigedia Jenerali Felix Kulayigye.

Wanajeshi wengine watatu waliokuwa kwenye ndege hiyo walinusurika lakini walipata majeraha makubwa, wakiwemo walioungua vibaya.

Kulayigye alisema kuwa ajali hiyo ilisababisha mlipuko wa risasi na silaha zilizokuwa ndani ya ndege, uliosababisha uharibifu wa majengo jirani na kuwajeruhi raia watatu.

AUSSOM ilithibitisha kuwa kazi za uokoaji na kuondoa mabaki ya ndege zilianza mara moja.

Mfanyakazi mmoja wa uwanja wa ndege, Farah Abdulle, aliambia shirika la Reuters: “Tuliskia mlipuko mkubwa, kisha tukaona moshi na moto ukipaa juu ya ndege.”

AUSSOM kwa sasa ina zaidi ya wanajeshi 11,000 nchini Somalia, waliopewa jukumu la kusaidia kuushinda kundi la al-Shabaab, ambalo lina uhusiano na al-Qaeda, na limekuwa likipambana na serikali halali ya Somalia kwa zaidi ya miaka 15.

Soma Izindi Nkuru

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *