Alhamisi tarehe 15 Mei, Seneti ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliunda kamati ya kiufundi kuchunguza uwezekano wa kumvua kinga ya kisheria rais wa zamani Joseph Kabila, ambaye ni seneta wa maisha, ili afikishwe mbele ya sheria.
Taarifa kutoka bungeni zinaonyesha kuwa kulikuwa na mgawanyiko wa maoni kuhusu suala hilo. Baadhi ya maseneta waliunga mkono kuondolewa kwa kinga hiyo, huku wengine wakisisitiza kuwa kulingana na Kifungu cha 224 cha kanuni za Seneti, lazima pawepo kura ya pamoja ya Bunge.
Kwa mujibu wa Radio Okapi, Seneti ilianza kushughulikia ombi la Mkaguzi Mkuu wa Jeshi la FARDC, linalotaka Kabila avuliwe kinga. Uchunguzi huo unaendeshwa kwa siri, kutokana na uzito wa suala hilo na nafasi ya Kabila kama rais wa zamani wa miaka 18.
Serikali ya Congo inamtuhumu Kabila kwa kuanzisha au kusaidia kundi la waasi la AFC/M23, linalopambana na serikali na kudhibiti maeneo makubwa ya Kivu Kaskazini na Kusini.
Rais huyo wa zamani, ambaye sasa yuko uhamishoni, anatuhumiwa kwa makosa makubwa: uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu, na mauaji ya raia.


