Katika hatua isiyokuwa ya kawaida, Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imetangaza kusitisha kwa muda shughuli zote za kisiasa za chama cha People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD), chama kilichoanzishwa na Rais wa zamani Joseph Kabila.
Uamuzi huo ulitiwa saini na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Jacquemain Shabani, kutokana na wasiwasi kuhusu usalama wa taifa, hasa kufuatia kuimarika kwa waasi wa M23 mashariki mwa nchi.
Katika hotuba yake, Shabani alimkosoa Kabila kwa “msimamo usioeleweka” mbele ya kile alichokiita “vita vinavyoongozwa na Rwanda”, akionyesha wasiwasi juu ya ukimya wake na kurejea kwake mjini Goma – mji uliodhibitiwa kwa kiwango kikubwa na waasi.
Serikali imedai kuwa usalama wa Kabila katika Goma unalindwa na wanajeshi wanaohusishwa na waasi wa M23, jambo ambalo limezua maswali kuhusu nafasi yake katika mzozo huo unaoendelea.
Kwa mujibu wa vifungu vya sheria namba 29, 30 na 31(b) vya sheria ya vyama vya kisiasa nchini DRC, serikali imeagiza kusitishwa kwa shughuli zote za chama cha PPRD kote nchini.
Kesi hiyo sasa iko mikononi mwa ofisi ya mwendesha mashtaka katika Mahakama ya Katiba kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hatua za kisheria.
Waziri Shabani alieleza kuwa ukimya wa Kabila ni sawa na kushirikiana na maadui, akisema kuwa hiyo ni kuvunja majukumu ya kisheria na kiadili ya viongozi wa kisiasa, hususan wale waliowahi kuwa marais na wanaheshimiwa kama maseneta wa kudumu.
Aliwakumbusha viongozi wa vyama vya siasa kuwa wanawajibika kulinda umoja wa kitaifa, mamlaka ya taifa, na uhai wa mipaka ya nchi.
Ingawa Kabila anadai kuwa amerudi nchini kusaidia kurejesha amani mashariki mwa Congo, maafisa wa Kinshasa wanasema kuwa kuwepo kwake huko kunazua maswali zaidi kuliko majibu.


