Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imetangaza kuwa itaiomba Uganda kutoa maelezo rasmi baada ya uamuzi wake wa kufungua mipaka inayoelekea kwenye maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa M23.
Wiki hii, Uganda ilifungua tena mipaka ya Bunagana na Ishasha, kufuatia agizo la Rais Yoweri Kaguta Museveni.
Kampala ilisema kuwa hatua hiyo ilikuwa ya kufufua biashara ya mipakani, ambayo imekuwa ikidorora tangu Juni 2022, wakati mipaka hiyo ilifungwa kutokana na mzozo wa M23.
Baada ya kikao cha baraza la mawaziri siku ya Ijumaa, msemaji wa serikali ya DRC, Patrick Muyaya, alisema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Thérèse Kayikwamba Wagner, amepewa jukumu la kuomba maelezo ya kina kutoka Uganda, kuhusu kwa nini walifungua mipaka bila uwepo wa mwakilishi yeyote kutoka serikali ya DRC.
Uganda imeeleza kuwa kufungwa kwa mpaka wa Bunagana kuliigharimu karibu shilingi milioni 500 za Uganda kwa mwaka, hasara kubwa ya kiuchumi ambayo ilisababisha hatua hiyo ya kufungua mipaka.


