Klabu ya APR FC imemfuta kazi kocha wake mkuu kutoka Serbia, Darko Novic, Jumanne tarehe 13 Mei.
Novic alianza kuifundisha timu ya jeshi ya Rwanda mwaka jana, akichukua nafasi ya Mfaransa Thierry Froger.
Ripoti zinaeleza kuwa uamuzi wa kumtimua ulifanyika Jumanne, ingawa klabu hiyo haijamjulisha rasmi kocha huyo ambaye alikuwa bado na mwaka mmoja kwenye mkataba wake.
Hivi karibuni, Novic aliiwezesha APR FC kushinda Kombe la Amani baada ya kuilaza Rayon Sports mabao 2-0 kwenye fainali. Hata hivyo, tangu alipowasili, mashabiki walikuwa wakilalamikia mbinu zake za ukocha.
Uamuzi huu unakuja wakati APR FC iko kwenye mbio kali za ubingwa dhidi ya Rayon Sports, huku zikiwa zimebaki mechi tatu kabla ya ligi kufungwa.
Klabu hiyo bado ina matumaini madogo ya kuchukua ubingwa, licha ya kutumia fedha nyingi kununua wachezaji wakati wa dirisha la usajili la kiangazi mwaka jana.


