Kamanda Mkuu wa Jeshi la Afrika Kusini (SANDF), Jenerali Rudzani Maphwanya, ametangaza kuwa wanajeshi wa taifa hilo wako tayari kurejea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupambana tena na kundi la waasi la M23, iwapo watahitajika.
Jenerali huyo alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wanajeshi wa Afrika Kusini waliokuwa wamerejea kutoka Goma na Mubambiro, ambapo walikuwa tangu Januari mwaka huu, baada ya kushindwa kwenye mapigano na M23 kuchukua mji wa Goma.
Jenerali Maphwanya aliwaambia wanajeshi wake kuwa hata M23 wenyewe walikiri kuwa SANDF iliwasababishia maumivu makali wakati wa mapigano ya Goma. Alisisitiza kuwa wako tayari kurudia hayo kama wakihitajika.
Alisema:
“Hadithi hii inaelezwa vizuri zaidi na waliokuwa upande mwingine wa uwanja wa vita, kwa sababu wanajua ukweli wake. Walisikia na walithibitisha wenyewe. Hivyo, tukihitajika kufanya tena—tutafanya. Na nitakuwa pamoja nanyi.”
Mapigano yaliyosababisha M23 kuteka Goma yalisababisha vifo vya wanajeshi 14 wa Afrika Kusini. Baada ya hapo, majeshi ya Afrika Kusini pamoja na yale ya Malawi na Tanzania hawakushiriki tena katika vita hadi waliporejea.
Jenerali Maphwanya aliwaambia wanajeshi wa SANDF kuwa ingawa wamerejea, yeye anawaona kama washindi—kwa sababu baada ya mapigano kusimama, wapinzani wao pamoja na serikali ya DRC walilazimika kukaa kwenye meza ya mazungumzo.


