Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) na Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) wamesaini mkataba mpya wa ushirikiano wa kijeshi siku ya Ijumaa.
Uwekaji saini huu ulifanyika wakati wa ziara ya Jenerali Muhoozi Kainerugaba jijini Kinshasa, ambaye ni Kamanda Mkuu wa Majeshi ya Uganda na mtoto wa Rais Yoweri Museveni.
Kwa mujibu wa FARDC, ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya majeshi ya pande mbili katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la ADF.
Katika kikao kati ya Jenerali Muhoozi na mwenzake wa DRC, Luteni Jenerali Jules Banza Mwilambwe, pande zote mbili zilisifu mafanikio yaliyopatikana katika oparesheni za pamoja, hasa katika Operesheni Shujaa inayolenga kulisambaratisha kundi la ADF.
Walieleza kuwa kambi nyingi za ADF tayari zimeweza kuharibiwa kupitia mashambulizi hayo ya pamoja.
FARDC na UPDF pia walisaini mkataba mwingine wa ushirikiano wa kijeshi, ukilenga kuratibu operesheni za kijeshi, kubadilishana taarifa za kiintelijensia, na kutoa mafunzo ya kijeshi, huku wakiheshimu uhuru wa DRC.
Ushirikiano huu wa kijeshi ulianza rasmi Novemba 2023, ambapo vikosi vya nchi hizo mbili vilianza mashambulizi dhidi ya ADF, na tayari wameweza kuwaua wapiganaji wengi wa kundi hilo, wakiwemo viongozi wao wakuu.


