Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila Kabange, anatarajiwa kutoa hotuba kwa wananchi Jumapili hii, tarehe 20 Aprili 2025, mjini Goma.
Kabila amekuwa mjini Goma tangu Ijumaa, baada ya kuwasili kutoka Harare, Zimbabwe alikokuwa akiishi tangu mwaka 2024.
Kabla ya kurejea nchini, Aprili 8, Kabila alitangaza kuwa anarudi nyumbani kutokana na hali mbaya ya usalama na kushindwa kwa taasisi za taifa, akisema anataka kusaidia kutafuta suluhisho.
Kwa sasa, DRC inakumbwa na hali tete ya usalama, hususan mashariki mwa nchi ambako mapigano yanaendelea kati ya jeshi la serikali na waasi wa M23.
Kabila ameituhumu serikali ya Rais Félix Tshisekedi kwa kuwa chanzo cha mzozo huo. Katika hotuba yake, anatarajiwa kueleza mwelekeo wa namna ya kulinusuru taifa.
Kiongozi huyo wa zamani wa DRC (2001–2018) atazungumza kutoka Goma, mji unaodhibitiwa kwa kiasi kikubwa na M23 – kundi la waasi ambalo pia lilimpinga wakati wa utawala wake kati ya 2012 na 2013.
Wakati huo huo, serikali ya Tshisekedi imetangaza kumfungulia mashitaka Kabila kwa tuhuma za usaliti mkubwa. Pia imetangaza kutaifisha mali zake zote na kusimamisha shughuli za chama chake cha PPRD-FCC.
Kabila anatarajiwa kuzungumzia mashtaka hayo katika hotuba yake.
Ripoti zinaashiria kwamba mwanasiasa mwingine maarufu wa upinzani, Moïse Katumbi, anaweza kuungana naye mjini Goma. Wawili hao walikutana mjini Addis Ababa, Ethiopia mwezi Desemba 2024, wakiahidi kushirikiana kulinusuru taifa lao.


