Katika mazungumzo ya amani yanayoendelea mjini Doha, Qatar, kati ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kundi la waasi la AFC/M23, imebainika kuwa moja ya madai makuu ya M23 ni kupewa mamlaka ya kuongoza majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini kwa kipindi cha miaka minane ijayo.
Mnamo Alhamisi, tarehe 10 Julai, Kinshasa na M23 walianzisha tena mazungumzo yaliyokuwa yamesimama, kwa upatanishi wa Qatar.
Kwa mujibu wa diplomatia mmoja wa DRC aliyezungumza na vyombo vya habari vya ndani, M23 inataka kupewa udhibiti kamili wa usalama, utawala na uchumi katika mikoa hiyo miwili muhimu.
“Wanaomba kupewa uongozi wa Kivu zote mbili,” alisema. “Wanataka mamlaka kamili juu ya usalama, utawala, na uchumi kwa miaka minane.”
Hata hivyo, serikali ya Congo imekataa vikali pendekezo hilo, ikisema kuwa litafungua njia kwa mpango wa muda mrefu wa kuigawanya Congo (Balkanization)—ambao Kinshasa inadai umeandaliwa na watu fulani kwa muda mrefu.
Serikali imesema kuwa hili ni suala nyeti lisilovumilika, na ni mstari mwekundu kwao.
Taarifa hii inakuja wakati ambapo AFC/M23 tayari imeanzisha mifumo ya utawala mbadala katika maeneo ya Kivu Kaskazini na Kusini na bado inashikilia maeneo muhimu ya mikoa hiyo.


