Kundi la waasi la M23 limeonyesha hasira kali baada ya Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwaita “wagonjwa wa akili.”
Jioni ya Jumatatu, tarehe 14 Julai, Waziri Dkt. Samuel Roger Kamba alisikika akisema kuwa wanachama wa AFC/M23 ni “wagonjwa wa akili wanaodhibiti sehemu za Kivu Kaskazini na Kusini,” wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mlipuko wa kipindupindu unaoikumba DRC.
Kauli hiyo ilitolewa wakati serikali ya DRC na kundi la AFC/M23 wakiendelea na mazungumzo ya amani huko Doha, Qatar, yanayolenga kumaliza vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu.
Katibu Mkuu wa AFC/M23, Benjamin Bonimpa, alilaani matamshi hayo, akisema ni kosa la heshima na linaonyesha kuwa serikali ya Kinshasa haina nia ya kweli kushiriki katika mazungumzo ya amani.
Alisema:
“Maneno haya ya matusi na ya kudhalilisha kutoka kwa viongozi wa Kinshasa dhidi ya wanachama wa AFC/M23, wakati mazungumzo ya Doha yanapiga hatua kubwa kuelekea amani, yanaonyesha kuwa serikali haina nia ya dhati na sisi tumelichukulia hilo kwa uzito.”
M23 bado haijatangaza hatua itakayochukua kufuatia tukio hilo.


