Kundi la waasi la M23 limetoa maelezo kuhusu maelfu ya miili iliyopatikana kwenye barabara za Goma kabla ya kuzikwa, likisema kuwa miili hiyo ni ya wanajeshi wa jeshi la serikali ya DRC na washirika wao waliouawa vitani.
Taarifa za hivi karibuni kutoka Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) zinaonyesha kuwa takriban miili 2,000 imekusanywa na kuzikwa kutoka barabara za Goma. Miili mingine 700 bado iko kwenye hifadhi ya maiti katika hospitali mbalimbali za jiji hilo, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Ripoti pia zinasema kuwa “kuna maiti nyingi zilizooza bado ziko katika maeneo mbalimbali, hasa kwenye uwanja wa ndege na karibu na gereza la Goma.”
Serikali ya DRC, kupitia Waziri wa Mawasiliano na msemaji wake Patrick Muyaya, hivi karibuni ilitangaza kuwa miili inayokusanywa Goma ni ya watu waliouawa na majeshi ya Rwanda, ingawa hakutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai hayo.
Kinshasa imekuwa ikizishutumu mara kwa mara majeshi ya Rwanda kwa kupigana bega kwa bega na waasi wa M23 dhidi ya jeshi lake la kitaifa, mara nyingi ikikanusha uwepo wa kundi la M23 kabisa.
Katika taarifa aliyoandika kwenye akaunti yake ya X, rais wa M23 alikanusha madai ya serikali ya Congo kuwa waliouawa ni raia, akisema kuwa miili iliyopatikana kwenye barabara za Goma ni ya wanajeshi wa serikali na washirika wao wa vita.
Alisema: “Utawala wa Kinshasa unapaswa kuacha kushiriki kwenye mijadala ya aibu kuhusu vifo vilivyotokea Goma. Miili iliyokuwa imejaa kwenye barabara za Goma ilikusanywa na mamlaka za afya na kuwekwa kwenye hifadhi ya maiti ya hospitali za Goma kabla ya kuzikwa. Kwa kweli, ni ya wanajeshi wa FARDC na washirika wao (Wazalendo, FDLR, FDNB na mamluki) waliouawa vitani.”
Bertrand Bisimwa alieleza kuwa baadhi ya wanajeshi wa FARDC na washirika wao waliopoteza vita walikataa kutii agizo la M23 la kuweka chini silaha zao kabla ya kukusanywa kwenye Uwanja wa Stade de l’Unité.
Aliendelea kusema: “Waliamua kupigana katikati ya jiji la Goma, jambo lililopelekea kuuawa kwao.”
M23 inasema kuwa miili ya wanajeshi hao tayari imezikwa, na sasa jiji la Goma liko salama kabisa.
Kundi hilo limeongeza kuwa hakuna familia yoyote inayoishi Goma iliyo kwenye maombolezo kwa kumpoteza mpendwa wao.


