Makundi mawili ya waasi ambayo zamani yalikuwa sehemu ya muungano uliotaka kumpindua Rais Faustin-Archange Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, yamekubali kuweka silaha chini na kujiunga na serikali.
Makundi ya Unité pour la Paix en Centrafrique (UPC) na Retour, Réclamation et Réhabilitation (3Rs), yaliyokuwa yenye nguvu zaidi katika muungano wa CPC (Coalition des Patriotes pour le Changement), yameamua kusitisha mapigano.
Mwisho wa mwaka 2020, CPC, iliyokuwa inamuunga mkono rais wa zamani François Bozizé, ilishambulia mji mkuu Bangui, lakini ikazuiwa na majeshi ya Rwanda yaliyotumwa kusaidia serikali chini ya makubaliano ya usalama.
Kwa mujibu wa Africa Intelligence, tarehe 10 Julai 2025, Ali Darassa, kiongozi wa UPC, na Jenerali Sende Abdelkader, anayejulikana kama “Bobo Bobo”, kiongozi wa 3Rs, watatangaza rasmi kuvunjwa kwa makundi yao katika hafla mjini Bangui.
Uamuzi huu umetokana na mazungumzo yaliyofanyika Chad kati ya viongozi hao wa waasi na serikali ya Touadéra, ambapo walifikia makubaliano ya amani.
Mwezi wa Aprili, Jenerali Henry Wanzet Linguissara, mshauri wa usalama wa rais, alieleza kwamba Rais Touadéra alimwagiza aende Ndjamena kukutana na Bobo ili kumshawishi kusitisha mapigano.
“Tumekuwa vitani kwa miongo mingi. Rais kama mtu wa amani alisema kundi la 3Rs lazima lisitishe vita. Kiongozi wao, Abdelkader ‘Bobo’, yupo Ndjamena, na niliagizwa kwenda kuzungumza naye.”
Aliongeza kuwa Rais Mahamat Idriss Déby Itno wa Chad alikubali na kusaidia kufanikisha mazungumzo hayo.
“Bobo wa 3Rs alikubali kujiunga na mchakato wa APPR na kuacha vita kuanzia siku ya kutiwa saini.”
Wakati mazungumzo hayo yakiendelea, Darassa wa UPC naye alijiunga na akaunga mkono mkataba huo wa amani.


