Monna Walda Kaneza, anayefahamika zaidi kwa jina la kisanii Mow Kanzie, mmoja wa wasanii maarufu wa kike nchini Burundi, amefunga ndoa na mchumba wake wa muda mrefu.
Harusi ya kisheria ilifanyika tarehe 23 Machi 2025, ikifuatiwa na sherehe za kitamaduni zilizofanyika mapema mwezi huo.
Mow Kanzie mwenye umri wa miaka 27, ambaye alikuwa mshindi wa pili kwenye mashindano ya Miss Burundi mwaka 2016, alionyesha furaha yake kupitia mitandao ya kijamii, akisema kuwa maisha yake yameanza ukurasa mpya.
Aliandika: “Tabasamu zaidi, huzuni chache… mapenzi mengi, chuki kidogo. Kuna mengi ya kushukuru.”
Ingawa ana shahada ya uzamili katika masuala ya benki, Mow Kanzie anapendwa sana kwa muziki wake, hasa miongoni mwa vijana.
Baadhi ya nyimbo zilizompa umaarufu ni “Hakuna Matata Remix”, “Only One”, na “Ndapfuha” aliyoimba na Kidum.


