“Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuunga mkono wananchi wa Congo wakati huu wa ukosefu wa usalama na mahitaji yanayoongezeka ya kibinadamu, hasa katika eneo la mashariki,” alisema Tom Fletcher, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya misaada ya kibinadamu, baada ya kukutana na viongozi wa kundi la waasi la AFC/M23 siku ya Alhamisi, tarehe 26 Juni, huko Goma (Kivu Kaskazini).
Mkutano huu na viongozi wa AFC/M23 ulifunga ziara ya siku mbili ya Tom Fletcher katika eneo la Kivu Kaskazini.
Baada ya kutembelea maeneo ambayo maelfu ya watu waliokuwa wakimbizi wamerejea katika maeneo ya Nyiragongo na Masisi (Kivu Kaskazini), pamoja na Minova katika eneo la Kalehe (Kivu Kusini), afisa huyo wa Umoja wa Mataifa alisema “ameona kwa macho yake mateso ya watu” wanaokumbwa na milipuko ya magonjwa na changamoto za usalama na misaada ya kibinadamu.
Akasema: “Mahitaji ni makubwa sana! Na kwa hivyo, dunia lazima iwaunge mkono watu wa Kongo, hasa katika wakati huu mgumu na changamoto nyingi.”
Kwa sasa Umoja wa Mataifa unakumbwa na upungufu wa fedha, jambo linaloathiri utoaji wa misaada.
Fletcher alisema: “Lakini bado tumejitoa, tumehusika, na bado tupo.”
Alisema alijadili na viongozi wa AFC/M23 kuhusu sheria za kimataifa za kibinadamu katika maeneo wanayoyatawala.
Pia walijadili masuala ya chakula, afya, makazi, ulinzi — hasa dhidi ya ukatili wa kijinsia — na usalama wa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu.


