Rais Paul Kagame amewasili Astana, Kazakhstan, kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Alipowasili, Rais alipokelewa uwanjani na mwenyeji wake, Rais Kassym-Jomart Tokayev.
Inatarajiwa kuwa Jumatano tarehe 28 Mei, Rais Kagame atafanya mkutano wa faragha na Rais Tokayev, kisha wawili hao watazungumza na waandishi wa habari.
Rais Kagame pia atatoa hotuba kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Astana (Astana International Forum), jukwaa kubwa la majadiliano duniani.
Ziara ya Rais Kagame imefuatia ile ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Balozi Olivier Nduhungirehe, ambaye aliwasili Kazakhstan kabla ya Rais.
Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Kazakhstan ilitangaza kuwa Waziri Nduhungirehe alikutana na mwenzake wa Kazakhstan, Murat Nurtleu.
Mawaziri hao wawili walijadili masuala muhimu kama siasa, uchumi, utamaduni, na ushirikiano wa kibinadamu.
Waziri Nurtleu alisema:
“Tunaliangalia Rwanda kama taifa rafiki na mshirika muhimu barani Afrika. Nina imani kwamba jitihada zetu za pamoja zitaifanya ziara ya Rais Kagame kuwa mwanzo mpya wa ushirikiano bora kati ya Kazakhstan na Rwanda.”
Ziara hii inatarajiwa kuleta makubaliano ya ushirikiano katika biashara, teknolojia, na ulinzi.
Rais Kagame alikutana na Rais Tokayev kwa mara ya kwanza Novemba mwaka jana huko Baku, Azerbaijan, na walijadili kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa faida ya watu wa mataifa yote mawili.
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Rwanda na Kazakhstan ulianza rasmi mwaka wa 2016 baada ya Rwanda kumteua mwakilishi wake nchini humo.
Mnamo Septemba 2024, wakati wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko New York, mawaziri Nduhungirehe na Nurtleu walisaini makubaliano ya kuondoa visa kwa raia wa pande zote mbili, kurahisisha usafiri.
Picha:

Rais Kagame alipokelewa uwanjani na Rais Tokayev.

Jumatano, atatoa hotuba kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Astana.



