Rais Faustin-Archange Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati yanasemekana kuwa chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa serikali ya Urusi ili asaini mkataba wa ushirikiano wa kijeshi na kundi la wanamgambo wa Africa Corps kutoka Urusi.
Kundi hilo, linalojulikana pia kama Russian Expeditionary Corps (REK), linasimamiwa moja kwa moja na serikali ya Urusi.
Kwa mujibu wa Africa Intelligence, shinikizo linaloongezeka kutoka Kremlin linaweza kumfanya Rais Touadéra kusaini mkataba huo kabla ya mwisho wa mwaka huu, huku wapiganaji wa kwanza wakitarajiwa kufika Afrika ya Kati majira ya joto.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi inaripotiwa kutaka kupeleka wanajeshi wa Africa Corps kuchukua nafasi ya wapiganaji wa kundi la Wagner waliokuwa nchini humo tangu mwaka 2017 — jambo linalochukuliwa kuwa chanzo kikuu cha shinikizo hilo.
Hata hivyo, Rais Touadéra anaonekana kuwa na mashaka, na anaendelea kuchukua muda kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.
Mnamo Januari mwaka huu, Rais Touadéra alikwenda Moscow na kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin, baada ya kukutana awali na Balozi wa Urusi huko Bangui.
Katika mazungumzo hayo, Touadéra alieleza wasiwasi kuhusu masuala ya haki na sheria iwapo atasaini mkataba na Africa Corps, kundi linalochukuliwa kuwa mpinzani wa Wagner.
Hata hivyo, Waziri Msaidizi wa Ulinzi wa Urusi, Lounos-Bek Evkourov, alipokuwa ziarani Afrika ya Kati mwezi Machi, alisisitiza kwamba serikali ya Bangui inapaswa kuachana na Wagner — jambo lililowaweka viongozi wa nchi hiyo kwenye njia panda.
Africa Corps inatarajiwa kuanza kazi rasmi nchini humo mwaka 2026, baada ya uchaguzi wa rais.
Ikiwa itatekelezwa, Afrika ya Kati itaungana na mataifa mengine ya ukanda wa Sahel ambayo tayari yamebadilisha kundi la Wagner kwa Africa Corps, hasa baada ya kifo cha kiongozi wa Wagner, Evgueni Prigozhin.
Wapiganaji wa Wagner waliopo nchini humo wanatarajiwa kuingizwa taratibu katika Africa Corps pindi shughuli za kundi hilo zitakapoanza rasmi.


