Rwanda imeorodheshwa miongoni mwa nchi 50 masikini zaidi duniani kulingana na pato la taifa kwa mtu (GDP per capita), kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na kuchapishwa na Visual Capitalist tarehe 24 Juni 2025.
Orodha hii inaeleza hali ya uchumi wa kila nchi, lakini hasa inaonyesha ni kiasi gani raia mmoja anaweza kuingiza kwa mwaka katika nchi hiyo.
Kati ya nchi 50, Rwanda ina pato la taifa kwa mtu la $1,237, na inashika nafasi ya 43 duniani. Ingawa nchi hii imepiga hatua katika maendeleo endelevu miaka ya hivi karibuni, takwimu hizi zinaonyesha kuwa bado kuna safari ndefu ya kuboresha maisha ya kila raia.
Haya ndiyo mataifa 10 masikini zaidi duniani:
-
Sudan Kusini – $251
-
Burundi – $490
-
Jamhuri ya Afrika ya Kati – $532
-
Malawi – $580
-
Madagaska – $595
-
Sudan – $625
-
Msumbiji – $663
-
DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) – $743
-
Niger – $751
-
Somalia – $766
Kwa sasa, Sudan Kusini ndiyo nchi masikini zaidi duniani, ikiwa na GDP kwa kila mtu isiyozidi $251 kwa mwaka.
Ripoti inaeleza kuwa matatizo kama ukosefu wa usalama, utawala mbaya, vita, kuyumba kwa uchumi, na ukosefu wa fursa za uwekezaji ni baadhi ya sababu kuu zinazokwamisha maendeleo ya nchi nyingi katika orodha hii, hasa zile za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Nchi nyingi zina idadi kubwa ya watu lakini uchumi wao ni mdogo. Kwa mfano, India, nchi ya nne kwa ukubwa wa uchumi duniani, inashika nafasi ya 50 kwenye orodha hii, ikiwa na pato la $2,878 kwa kila mtu.
Bara la Afrika lina asilimia 19 ya watu wote duniani, lakini pato la bara zima linachangia asilimia 3 tu ya uchumi wa dunia unaokadiriwa kuwa na jumla ya trilioni $113.
Ingawa takwimu hizi zinaonyesha hali ya jumla ya uchumi, pato la taifa kwa mtu (GDP per capita) halionyeshi jinsi utajiri unavyogawanywa ndani ya nchi. Baadhi ya nchi zina GDP ya juu lakini pia zina pengo kubwa la kipato kati ya matajiri na masikini.


