Gq7r5AjWAAAh-mT

Salva Kiir Yuko Hai: Serikali ya Sudan Kusini Yakanusha Taarifa za Kifo

Sangiza iyi nkuru

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Kusini imekanusha vikali uvumi ulioenea kwenye mitandao ya kijamii unaodai kuwa Rais Salva Kiir Mayardit amefariki dunia.

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi, serikali ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki imethibitisha kuwa habari hizo ni za uongo na zinalenga kusambaza taharuki na wasiwasi. Imeeleza kuwa Rais Kiir yuko hai, ana afya njema, na anaendelea kutekeleza majukumu yake kama kiongozi wa taifa.

“Tunasema kwa msisitizo kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Sudan Kusini inakanusha vikali uvumi unaoendelea kusambazwa katika mitandao ya kijamii kwamba Mheshimiwa Rais Salva Kiir Mayardit amefariki dunia,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

“Tunataka kuwahakikishia raia wote wa Sudan Kusini, kanda hii na jumuiya ya kimataifa kwamba Rais Salva Kiir Mayardit yuko hai, ana afya nzuri na anaendelea kutekeleza majukumu yake ya kitaifa kikamilifu,” taarifa iliendelea kusema.

Serikali pia imelaani kwa nguvu ueneaji wa uvumi huu wa uongo, ikisema ni jaribio la makusudi kuvuruga utulivu wa taifa.

“Wizara inalaani vikali usambazaji wa habari hizi za uongo ambazo zinalenga kuchochea taharuki isiyo na msingi, mkanganyiko na kuvuruga amani ya taifa. Taarifa hizi feki zinawasaidia tu wale wenye nia ya kuhujumu mshikamano wa kitaifa, amani tuliyopigania na maendeleo endelevu ya nchi yetu,” taarifa iliongeza.

Sudan Kusini ilipata uhuru mwaka 2011 lakini imekumbwa na changamoto nyingi za kisiasa, hasa mzozo kati ya Rais Salva Kiir na aliyekuwa Makamu wake, Dkt Riek Machar Teny.

Licha ya changamoto hizo, serikali ya Sudan Kusini imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuboresha maisha ya wananchi na kutekeleza wajibu wake kama serikali.

Soma Izindi Nkuru

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *