Serikali ya Rwanda imethibitisha rasmi kuwa Rais Paul Kagame hajaumwa, kinyume na uvumi ulioenea kwenye mitandao ya kijamii hivi karibuni.
Kwa wiki kadhaa zilizopita, wapinzani wa serikali ya Rwanda pamoja na baadhi ya raia wa Congo wamekuwa wakieneza taarifa kuwa Rais anaumwa, huku wengine wakieneza uvumi kuwa tayari amefariki.
Wanaosambaza uvumi huu wanasema kuwa Rais Kagame hajaonekana hadharani kwa takriban wiki tatu. Mara ya mwisho alionekana mnamo Juni 6, alipokuwa akipokea ujumbe kutoka Shule ya Hope Haven Christian ukiongozwa na Susan Hollern.
Tofauti na uvumi huo, Serikali imesema kuwa Rais yuko salama kabisa na kwamba kutokuonekana kwake hadharani ni kwa sababu alikuwa akipumzika.
Msemaji wa serikali, Yolande Makolo, aliliambia gazeti la Taarifa kuwa madai kuwa Rais anaumwa hayana msingi wowote na kuwataka Warwanda watulie.
Alisema: “Tafadhali msikubali kupotoshwa na taarifa hizi za chuki zisizo za kweli. Hakuna la kuogopa wala kuhofia.”
Makolo aliongeza kuwa ni jambo la kawaida kwa Rais kutokuonekana kwa muda mfupi, hasa baada ya kazi nyingi za kitaifa na kimataifa.
“Yeye pia ni binadamu, na kama wengine, anahitaji muda wa kupumzika. Hakuna la kushangaza wala hatari. Rais yuko salama na bado yuko kazini kama kawaida,” aliongeza.
Sio mara ya kwanza uvumi kuhusu afya ya Rais kuenea. Hapo awali, Rais mwenyewe amewahi kukanusha habari kama hizo.
Serikali imesema uvumi huu unasababishwa na sababu za kisiasa.


