Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa amesikitishwa na mwenendo wa Rais wa Urusi Vladimir Putin katika vita ya Ukraine, lakini hajakata tamaa kabisa ya kufanya mazungumzo naye.
Akizungumza na BBC, Trump alisema kwamba aliwahi kuamini kuna nafasi ya kumaliza vita hiyo, lakini mambo yaliharibika kila mara. Alisema:
“Tulikuwa karibu kufikia makubaliano mara nne tofauti, lakini kila mara yalifuatiwa na mashambulizi mapya.”
Matamshi haya yanakuja baada ya kutangaza msaada mpya wa silaha kwa Ukraine, na pia kuweka muda wa karibu miezi miwili kwa Urusi kutuliza hali — la sivyo ikabiliwe na vikwazo vikali vya kiuchumi.
Trump, ambaye hapo awali alikosoa NATO, sasa anasema anaiona kama shirika lenye nguvu na dhamira ya kujilinda:
“NATO sasa inalipa michango yake na inasonga mbele kwa nguvu.”
Pia alikumbuka jaribio la kuuawa lililotokea mwaka jana huko Pennsylvania, akisema hataki kufikiria jinsi lilivyomwathiri kwani ni tukio linalobadilisha maisha kabisa.
Trump alisisitiza kuwa anaendelea kufanya kazi ya kuwarejesha wahamiaji waliovuka mipaka kinyume cha sheria, akisema maelfu tayari wamerejeshwa El Salvador na nchi nyingine za Amerika ya Kusini.
Hatimaye, alitangaza kuwa atafanya ziara rasmi ya pili nchini Uingereza mwezi Septemba, ambako atakutana na Mfalme Charles III, na kusema anamuheshimu sana.
Tangazo hili linakuja wakati Urusi imeongeza mashambulizi ya drone na makombora kwenye miji ya Ukraine, ambapo raia ndio wanaoathirika zaidi. Kwa upande wake, Putin anasema anataka amani, lakini lazima sababu za msingi za vita zitatuliwe kwanza.


