Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza kwamba ndani ya wiki mbili zijazo atawakaribisha Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais Félix Antoine Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika Ikulu ya White House.
Viongozi hao wawili watapokelewa kufuatia mkataba wa ushirikiano uliosainiwa kati ya Rwanda na DRC mnamo tarehe 27 Juni.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana usiku, Trump alisema kuwa mkataba huo unalenga kumaliza mgogoro aliouelezea kuwa umeendelea kwa miaka 30 kati ya Rwanda na Kongo.
“Tarehe 27 Juni, mawaziri wa mambo ya nje wa DRC na Rwanda walikuja White House kusaini mkataba wa kihistoria wa amani tuliokuwa tumekubaliana,” alisema Trump.
Akaongeza:
“Walikuwa wakipigana kwa miaka 30. Watu milioni 7 walifariki, na wengine wanadai idadi halisi ni kubwa zaidi. Ulikuwa mgogoro wa muda mrefu na wa maafa makubwa.”
Trump alisema kwamba katika kipindi cha wiki mbili zijazo, atawakaribisha Kagame na Tshisekedi kukamilisha rasmi makubaliano hayo.
Mkataba huo uliosainiwa tarehe 27 Juni unaitaka Kinshasa kuvunja kundi la kigaidi la FDLR.
Pia unasisitiza ushirikiano wa kiuchumi kati ya Rwanda na DRC, hasa katika sekta ya madini.


