Mwendesha mashtaka nchini Ubelgiji amepokea kesi inayowahusisha baadhi ya watu kutoka familia ya Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakituhumiwa kuiba madini ya thamani katika majimbo ya Haut-Katanga na Lualaba.
Ripoti zinaeleza kuwa malalamiko hayo yaliwasilishwa na wanasheria Bernard Maingain na Brieuc kwa mwendesha mashtaka Ann Fransen mnamo tarehe 8 Julai 2025.
Wanafamilia wa Tshisekedi wameshtakiwa nchini Ubelgiji kwa sababu wana uraia wa huko. Miongoni mwao ni ndugu yake Rais, Christian Tshisekedi, anayeshutumiwa kuchukua kwa nguvu maeneo mengi ya machimbo ya madini huko Katanga, na kuweka wanajeshi wa kulinda maeneo hayo kila wakati.
Walalamikaji pia wamezitaka asasi zisizo za kiserikali zinazofanya kazi katika mikoa ya Haut-Katanga na Lualaba, pamoja na viongozi wa zamani wa Gécamines (kampuni ya taifa ya madini) kushughulikia suala hilo.
Mkuu wa chama cha wachimbaji madini katika Lualaba alisema:
“Tangu mwaka 2019, mambo yameharibika kabisa. Katanga imekuwa kama sanduku la pesa la familia hiyo katika majimbo haya, hasa Lualaba, bila hata uwekezaji wowote kutoka kwao.”
Mbali na kaka wa Rais, malalamiko hayo pia yanamgusa mke wa Rais, Denise Nyakeru, mwana wao Anthony Tshisekedi, pamoja na binamu zake na shemeji yake.


