Wapiganaji kutoka kwa makundi ya silaha ambayo Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) huwaita Wazalendo, wanadaiwa kuwateka nyara maafisa wawili wa ngazi ya juu wa kundi la waasi la M23.
Maafisa hao walikuwa wakiongoza vikosi vya M23 katika eneo la Misinga, katika Groupement ya Ikobo, Wilaya ya Walikale.
Kwa mujibu wa ACTUALITÉ, utekaji huo ulitokea usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu, tarehe 30 Juni, wakati walikuwa safarini kati ya vijiji vya Kirumburumbu na Muuli.
Watu waliotoa taarifa kwa chombo hicho cha habari hawakutoa majina ya maafisa waliotekwa, lakini walisema walichukuliwa hadi katika kituo kikuu cha Wazalendo kinachoitwa Buhimba.
Kundi la M23 halijatoa taarifa yoyote kuhusu tukio hilo.
Ripoti nyingine zinaeleza kuwa Jumatatu, wapiganaji wa M23 walifanya operesheni ya msako katika misitu ya Kirumburumbu na Muuli ili kuwasaka watekaji, lakini hawakuwapata.
Hadi kufikia jioni ya Jumatatu, hakukuwa na taarifa mpya kuhusu hali ya maafisa waliotekwa.


