Katika chumba cha mahakama ya Rufaa ya Huye, siku ya Jumatatu tarehe 7 Julai, kesi ya watu watano, wakiwemo mwanamke mmoja, ilisikilizwa ambapo wanatuhumiwa na upande wa mashtaka kwa kumuua mwanaume mwenye umri wa miaka 57 kwa kumkata koo.
Uhalifu huo ulitokea usiku wa tarehe 7 Juni 2025, majira ya saa nne usiku, katika kijiji cha Ngoma III, kata ya Ngoma, sekta ya Ngoma, wilaya ya Huye, ambapo marehemu alipatikana amekufa ndani ya nyumba yake.
Kulingana na taarifa kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu, washtakiwa walikiri makosa yao mahakamani na kueleza jinsi walivyopanga mauaji hayo: walitengeneza funguo bandia za nyumba aliyokuwa akiishi marehemu, kisha jioni walimvizia aliporudi nyumbani. Alipoingia tu, walimkamata, wakamkaba koo huku wengine wakimshika miguu, mmoja wao akachukua kisu na kumkata koo hadi kufa. Walitubu na kuomba msamaha kwa kitendo hicho.
Mwendesha mashtaka aliomba hukumu ya kifungo cha maisha kwa washukiwa wanne, kwa mujibu wa kifungu cha 107 cha Sheria Na. 68/2018 ya tarehe 30/08/2018 kuhusu makosa na adhabu kwa ujumla. Mtuhumiwa wa tano, aliyeficha taarifa baada ya kujua kuwa marehemu atauwawa, alipendekezewa kifungo cha miaka miwili na faini ya faranga 500,000 za Rwanda.
Kesi ilifungwa, na uamuzi utasomwa tarehe 21 Julai 2025 saa tisa alasiri.


