Nchini Uganda, uamuzi wa serikali kupeleka wanajeshi DRC una utata. Chama kikuu cha upinzani, FDC siku ya Jumanne kilimwomba rais kuwaeleza Waganda faida za kutumwa huku .
Wanajeshi elfu mbili wa Uganda watatumwa mashariki mwa DRC chini ya bendera ya jeshi la kanda ya Afrika Mashariki, lenye jukumu la kusimamia uondoaji wa waasi wa M23. Wanajeshi wa Uganda hawapo kwa ajili ya “kupambana” na M23, anasisitiza Kampala, lakini kuchukua, kama kikosi “kisichofungamana na upande wowote”, nafasi zilizoachwa na vuguvugu la waasi.
Hoja ambayo haikiamini kabisa chama kikuu cha upinzani. Kwa upinzani, ni juu ya mtazamo mbaya wa Uganda machoni pa Wakongo ambao unaitia wasiwasi. “Uganda na Rwanda zimeshutumiwa na wakazi wa Kongo kwa kuunga mkono vuguvugu la M23. Kutuma wanajeshi wa Uganda nchini humo kunawaweka hatarini. Unapopigana na adui na watu walio nyuma yako pia kukushambulia, inaweza kugharimu maisha ya wanajeshi wengi wa Uganda,” anahofia Fungaroo Kaps Hassan, katibu wa kitaifa wa FDC.
Uganda tayari ina mamia ya wanajeshi nchini DRC, waliotumwa mwaka 2021 kupigana na waasi wa ADF. Kampala pia iliingilia kati Kongo katika miaka ya 1990 wakati wa Vita vya Pili vya Kongo, na lazima sasa kulipa fidia kwa uharibifu uliosababishwa na wanajeshi wake.
Hivyo, Fungaroo Kaps Hassan anahofia dimbwi jipya la fedha kwa nchi. “Walipakodi wa Uganda bado hawajamaliza kurejesha pesa zilizoporwa katika vita vya awali na serikali inataka kutuma wanajeshi zaidi Kongo ili kuunda mazingira mapya ya uporaji? Tunataka maelezo ya wazi kutoka kwa Rais Museveni ili kuhalalisha kutumwa huku. Wanajeshi wa Uganda lazima wasiwe mali yake binafsi,” alisema.
Wasimamizi kadhaa wa FDC watakutana Jumatano hii katika jimbo la West Nile kwenye mpaka na DRC kuandaa hoja katika Bunge dhidi ya uingiliaji kati wa Uganda nchini DRC. Mkutano ambao unaenda sambamba na ziara ya Rais Museveni mkoani humo.


