Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa Pelé, raia wa Brazil, ndiye mchezaji bora zaidi wa soka kuwahi kuishi.
Kauli hiyo aliitoa baada ya fainali ya Kombe la Dunia la Klabu ambapo Chelsea (Uingereza) iliibuka mshindi dhidi ya Paris Saint-Germain (Ufaransa) kwa mabao 3-0, katika Uwanja wa MetLife mbele ya mashabiki zaidi ya 81,000.
Trump pamoja na Rais wa FIFA Gianni Infantino waliwasilisha kombe hilo kwa Chelsea.
Akizungumza na televisheni ya DAZN, Trump alisema:
“Miaka mingi iliyopita nilipokuwa kijana, walimleta mchezaji aitwaye Pelé achezee timu iitwayo Cosmos. Uwanja ulikuwa umejaa kabisa, kama ilivyo leo, yote ni kwa sababu ya Pelé.”
“Sikumbuki kila kitu vizuri kwa sababu nilikuwa mdogo, lakini nakumbuka kwenda kumtazama Pelé. Alikuwa wa ajabu. Kwa hivyo nikitazama nyuma, nasema Babe Ruth na Pelé walikuwa magwiji wa kweli.”
Pelé alifariki dunia mwaka 2022, na alichezea timu kadhaa zikiwemo New York Cosmos kati ya 1975 na 1977 kabla ya kustaafu.
Mbali na Pelé, wachezaji wengine wanaotajwa kuwa bora wa wakati wote ni pamoja na Lionel Messi, Diego Maradona, Zinedine Zidane, Ronaldinho, Ronaldo Nazário, na Cristiano Ronaldo.


