DRC Yasema Kabila Anachunguzwa Kwa Kutoroka Hadi Rwanda Bila Idhini
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imesema kuwa moja ya sababu inazomchunguza rais wa zamani Joseph Kabila Kabange ni kwa madai kuwa alisafiri kwa siri kuelekea Rwanda.
Mwezi uliopita, Kabila ambaye ameishi uhamishoni kwa muda, alitangaza nia ya kurejea DRC kupitia mashariki mwa nchi hiyo.
Siku chache baadaye, ripoti zilidai kuwa alikuwa Goma tangu Januari mwaka huu. Hili lilipelekea serikali ya Kinshasa kuchukua hatua kali: kumfungulia mashtaka, kusitisha shughuli za chama chake cha PPRD, na kugandisha mali zake zote.
Mnamo Aprili 24, Waziri wa Mambo ya Ndani Jacquemain Shabani alitoa taarifa kwa Mwanasheria Mkuu wa Mahakama ya Katiba, akitaka Kabila achunguzwe rasmi. Alisema haikuwa sahihi kwa rais wa zamani kusafiri kwenda Rwanda au maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa M23 bila idhini ya serikali.
Akasema: “Kama kiongozi wa zamani wa nchi, hakupaswa kusafiri kwenda Rwanda au maeneo yaliyovamiwa bila vyombo vya serikali kufahamu. Kifungu cha 5 cha Sheria Na. 18/021 ya Julai 26, 2018 kuhusu marais wastaafu waliochaguliwa kinamtaka azingatie heshima, uzalendo na uaminifu.”
Hadi sasa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha kuwa Kabila alienda Rwanda au Goma, na hakuna picha zinazoonyesha uwepo wake huko. Chama chake cha PPRD kimekanusha madai hayo.
Baada ya tetesi hizo, Kabila alionekana mjini Mbabane nchini Eswatini, akihudhuria sherehe ya siku ya kuzaliwa kwa Mfalme Mswati III.


