Ndege zisizo na rubani kutoka Ukraine zilifanya shambulizi usiku katika eneo la Kursk, Urusi, na kuharibu hospitali na majengo ya makazi ya ghorofa, huku mtu mmoja akijeruhiwa, kwa mujibu wa taarifa ya gavana wa mkoa huo Ijumaa asubuhi.
Mpaka upande wa pili, katika eneo la Sumy nchini Ukraine, gavana wa eneo hilo aliripoti mapigano mapya katika vijiji vilivyo karibu na mpaka, ambapo majeshi ya Urusi yanachukua maeneo. Alisema kuwa baadhi ya sehemu za mkoa wake huenda zikaangukia mikononi mwa Urusi.
Rais wa Urusi, Vladimir Putin, alisema kuwa anataka kuanzisha eneo huru (buffer zone) katika mkoa wa Sumy, ambao hapo awali ulitumika na Ukraine kuingia Kursk mwaka uliopita.
Katika mkoa wa Kursk—ambapo jeshi la Urusi lilidai kuwazuia wanajeshi wa Ukraine Agosti mwaka jana—Gavana Alexander Khinshtein alisema droni za Ukraine zilishambulia tena mji wa Kursk.
Kupitia ukurasa wake wa Telegram, Khinshtein alisema: “Vipande vya droni viliharibu hospitali kuu ya jiji la Kursk. Madirisha yalivunjika. Kwa bahati nzuri, hakuna mgonjwa aliyejeruhiwa.” Aliongeza kuwa vipande hivyo pia viliharibu majengo ya ghorofa.
Kwa upande mwingine, jeshi la Ukraine lilithibitisha kuwa linaendelea kufanya operesheni katika maeneo madogo ya mkoa wa Kursk, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Katika mkoa wa Sumy, ambao umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara na Urusi kwa miezi kadhaa, viongozi walisema wiki hii kwamba majeshi ya Urusi sasa yanadhibiti angalau vijiji vinne vya mpakani.
Gavana Oleh Hryhorov aliandika katika ukurasa wake wa Facebook: “Mapigano makali yanaendelea katika maeneo fulani, hasa karibu na vijiji vya Khotyn na Yunakivka.”
Alhamisi, Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilitangaza kuwa majeshi yake yaliteka vijiji vitatu zaidi huku yakisonga polepole mashariki mwa Ukraine.


