Rais Paul Kagame ametoa onyo kali kwa Rais Félix Antoine Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambaye aliwahi kutishia kushambulia Rwanda kwa kutumia drones na makombora ya masafa marefu. Kagame alisema wazi kuwa endapo mashambulizi hayo yatatokea, Rwanda itamfuata Tshisekedi hadi mahali anapotokea kuyapiga.
Mwaka wa 2023, Tshisekedi akiwa kwenye kampeni za urais, alimtuhumu Kagame kwa kuisaidia kundi la waasi la M23, na akatishia kulipiza kisasi kwa kushambulia Rwanda.
Katika hotuba yake huko Sainte-Thérèse mjini Kinshasa, aliwaambia raia wake:
“Msiogope. Jeshi letu linaweza kushambulia Kigali kutoka Goma. Kagame hatalala tena nyumbani kwake, atalala msituni. Ajaribu kucheza na wengine, lakini siyo na Fatshi Béton.”
Tshisekedi alisisitiza kuwa FARDC ina drones na makombora ya kufikia Kigali, na kuongeza:
“Risasi moja ikirushwa kutoka Rwanda kuja Goma au sehemu nyingine yoyote, nitaomba ruhusa ya Bunge kutangaza vita dhidi ya Rwanda.”
Lakini sasa, mji wa Goma ambao alikuwa akiuzungumzia, umechukuliwa na waasi wa M23 kwa zaidi ya miezi mitano tangu Januari 2025, baada ya kuwaondoa wanajeshi wa serikali.
Katika hotuba yake Ijumaa usiku kwenye sherehe za Siku ya Ukombozi zilizofanyika Kigali Convention Center, Kagame alisema:
“Mmekuwa mkisikia watu wakijivunia kuwa na nguvu, kuwa na drones, makombora, wakisema wanaweza kusababisha matatizo katika mji huu kutoka mbali. Tuliwaambia—hata kama hatuna hayo yote, tutajua tuwafuate walipo.”
Akaongeza:
“Tuna uwezo ambao hamjui. Tunaweza kusafiri zaidi ya kilomita 2,000 tukipigana kama ni lazima. Mengine ni maneno tu. Wale wanaodai kuwa na drones na silaha nyingine na kwamba wataishambulia Rwanda—tutawafuata hadi kwenye maeneo wanapotokea kuyapiga.”


