Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Kinshasa, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kardinali Fridolin Ambongo, amesema hana imani na mkataba wa amani ulioingiwa kati ya DRC na Rwanda.
Kardinali Ambongo aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Roma, Italia.
Mnamo tarehe 27 Juni, Rwanda na DRC zilitia saini mkataba wa amani wenye lengo la kumaliza miaka zaidi ya 30 ya mizozo kati ya mataifa hayo mawili.
Mkataba huo ulifanikishwa kwa usaidizi wa Marekani, na Rais Donald Trump aliuita kuwa wa kihistoria, akisema unalenga kumaliza kabisa vita kati ya DRC na Rwanda.
Hata hivyo, Kardinali Ambongo, ambaye ni sauti yenye ushawishi mkubwa nchini DRC, alisema mkataba huo ni “suluhisho la uongo” kwa migogoro inayoendelea kwa miongo kadhaa mashariki mwa DRC.
Alisema hana imani na njia ya Trump, kwani tayari alishindwa kuleta amani kati ya Ukraine na Urusi.
“Mlivyosikia hivi majuzi, Trump anasema ataleta amani kati ya DRC na Rwanda. Vita ni kwa sababu ya madini, halafu anasema ‘mimi Trump ninakuja kusuluhisha, lakini nitoeni madini’. Aliwahi kujaribu hili Ukraine na haikufanikiwa. Huku kwetu, ukisema jina lake tu, watu wanakimbia kwa hofu.”
Aliongeza kuwa utaratibu uliotumika kusaini mkataba huo haukubaliki na umepitwa na wakati.
“Tunaweza kusema kuwa haya masharti na mchakato mzima sasa yametosha. Suluhisho bandia yamezidi. Maamuzi kuchukuliwa bila kuwasikiliza walioathirika na ukosefu wa usalama yamekuwa ya kuchosha.”
Mkataba huo wa amani unaotiliwa shaka na Ambongo unahusisha mambo muhimu kama vile kuvunjwa kwa kikundi cha waasi cha FDLR, ambacho kwa zaidi ya miaka 30 kimekuwa kikihusishwa na machafuko mashariki mwa DRC.
Pia, unabainisha kuwa mzozo na kundi la M23, ambalo limekuwa likipigana na serikali ya DRC kwa takriban miaka minne, unapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo yanayoendelea mjini Doha, Qatar.


