Kundi la waasi la M23 limetangaza kuwa watu 874 wamethibitishwa kufariki katika mapigano yaliyowezesha kundi hilo kuuteka mji wa Goma mwezi Januari mwaka huu.
Taarifa hiyo ilitolewa siku ya Jumatatu katika mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa na kundi hilo.
Mwezi Januari, M23 ilichukua udhibiti wa Goma baada ya kufukuza ushirika wa majeshi uliokuwa na wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC), FDLR, wanajeshi wa Burundi, wanajeshi wa SADC, wanamgambo wa Wazalendo na mamluki weupe.
Baada ya kuteka mji huo, mashirika mbalimbali yakiwemo Amnesty International yalimtuhumu M23 kwa kufanya mauaji ya halaiki huko Goma, yakidai kuwa zaidi ya watu 3,000 waliuawa.
Delion Kimpulumpu, Katibu Mkuu wa muungano wa AFC unaojumuisha M23, aliwaambia waandishi wa habari kuwa madai hayo dhidi ya M23 “hayana msingi wowote.”
Alisema: “Idadi ya vifo 3,000 iliyotajwa na Kinshasa inaonekana kuwa ya kupindukia.”
M23 ilisema kuwa kati ya tarehe 2 hadi 13 Februari, miili 874 ilipatikana Goma kabla ya kuzikwa.
Rais wa kundi hilo, Bertrand Bisimwa, alisema kuwa “zaidi ya 90% ya waliokufa walikuwa wapiganaji,” wakiwemo wanachama wa AFC/M23, wanajeshi wa muungano wa serikali na wapiganaji wengine waliokuwa na silaha.
Pia M23 ilikanusha kuhusika na tukio la asubuhi ya tarehe 27 Januari, ambapo baadhi ya wafungwa wa gereza la Munzenze walitoroka na kuwachoma moto wenzao. Walisema tukio hilo lilitokea kabla ya jeshi lao kuingia Goma.
Kundi hilo pia liliishtumu serikali ya DRC kwa kuendelea kufanya kila juhudi kuhujumu usalama wa miji ya Goma na Bukavu, pamoja na maeneo mengine inayoyadhibiti.


