Watu wawili walipigwa risasi katika eneo la msitu wa Nyungwe, haswa katika kijiji cha Ntendezi, kata ya Ruharambuga, wilaya ya Nyamasheke. Mmoja alikufa na mwingine alijeruhiwa.
Polisi ya Rwanda ilieleza kuwa wawili hao walikuwa miongoni mwa kundi la watu 15 waliokuwa wameingia msituni wakiwa na mbwa na silaha za jadi, wakishukiwa kuwa na nia ya kuchimba madini kinyume cha sheria.
Kupitia ukurasa wake rasmi wa X (zamani Twitter), Polisi iliandika:
“Usiku uliopita karibu saa 10:30 alfajiri, watu 15 wakiwa na silaha za jadi na mbwa waliingia katika msitu wa Nyungwe, wakishukiwa kufanya uchimbaji wa madini usio halali.”
Ikaendelea kusema:
“Waliposimamishwa na walinzi wa msitu, walikataa kutii, wakawazunguka na kuanza kupambana nao. Hapo ndipo wawili walipigwa risasi, wengine wakakimbia.”
Kulingana na Polisi, waliopigwa risasi walikimbizwa katika hospitali ya Bushenge, lakini mmoja wao alifariki dunia baadaye.
Jeshi la Polisi lilitoa pole kwa familia ya marehemu na likaongeza kuwa uchunguzi juu ya tukio hilo umeanza.


